Nadhani hii mada nishaizungumzia kabla lakini kwakua kuna mtu kaniuliza naomba nirudie tena, kama mwanaume hajakuoa ni mpenzi wako tu au mchumba unatakiwa kujua kuwa si mume wako hivyo maisha yake hayakuhusu hata kwa sekunde moja. Anaweza kukuacha wakati wowote na wala hata pata dhambi yoyote hata kama mlitumia miaka kumi katika uchumba, narudia mapenzi yanaweza kuisha wakati wowote na akawa na haki ya kuondoka!
Sasa kuna tabia moja ambayo mwanamke akimpenda mwanaume, akiwa naye muda mrefu katika mahusiano au hata ni muda mfupi anataka kumshauri na kuchukua majukumu ya mke. Mwanamke unaanza kujiozesha kwa mwanaume kwa kuanza kumshauri kuhusu maisha yake. Tena kumbuka hapa si kwa ubaya lakini ni kama unataka umbadilishe yule mwanaume kuwa unavyotaka wewe.
Umemkuta mwanaume ni mlevi unakazana aache pombe, kila siku akilewa ni kulalamika, kila siku mnagombana kuhusu pombe, umemkuta anapenda starehe unaanza kumshauri kuhusu kujenga, unampangia mambo ya maendeleo na kila kitu. Umekuta anasomesha ndugu zake, wanakua kama wanamchuna unataka kumbadilisha na kutaka awekeze kidogo asiendekeze marafiki na mambo mengine kama hayo.
Ushauri wote huu ni mzuri na hujafanya kitu kibaya kumshauri lakini wakati unamshauri unatakiuwa kukumbuka kuwa wewe si mkewe hivyo kazi yako pekee ni kushauri tu. Huna haki ya kulalamika kila siku kua hakusikilizi, kulia kuwa hataki kubadilika, kumsumbua kuwa anaharibu maisha yake. Haki yako ni kushauri tu narudia kushauri hivyo anaweza kuamua kuchukua ushauri wako au kuachana nao na huna haki ya kulalamika.
Nataka mnielewe hapa, unachofanya ni kitu kizuri kama mpenzi una malengo naye unapaswa kufanya hivyo hasa kama mhusika ni kama hajielewi. Lakini kosa lako ni kule kulazimishia afanye hata kama ni mambo ya maendeleo. Kwamba unanuna eti hataki kujenga, unanuna eti hataki kuacha pombe, unanuna eti hataki kuacha umalaya, hapana kumbuka hayo ni maisha yake kachagua ndiyo furaha yake.
Sasa kama umemchagua unampenda unapaswa kumpenda hivyo hivyo na si kutaka kumbadilisha. Sijui hapa mnanielewa, si kitu kibaya, ni kwa manufaa yake, lakini ni yake hivyo kama hataki ni hataki, ni maisha yake hayakuhusu, wewe si ndugu yake, si Mama yake, si mke wake hivyo kama unaona hakufai nenda tafuta mwingine anayekufaa. Kama hataki kubadilika ondoka tafuta ambao hawahitaji kubadilishwa.
Unachotakiwa kufanya ni kumshauri na kama hatafuata ushuri wako basi achana naye au endelea naye kama alivyo, ukizidi kulazimishia ni kama unataka kumtawala na kumpangia maisha ambayo hayakuhusu. Kama ni mambo ya maendeleo, unataka mwanaume anayewaza kujenga katafute, kama hutaki mlevi katafute, kama hutaki Malaya katafute. Unachotaka wewe ni kwenda hotelini ukaagiza ugali halafu unataka ladha ya wali.
Hapana, unaposhauri na kutaka kulazimisha, kununa kwakua ushauri wako haufuatwi basi hapo huwi mshauri unakua kama bosi eti kwakua hutaki mlevi aache pombe! Yaani aache pombe kukuridhisha wewe! Aache kwakua anakupenda na anataka kuacha lakini si kwakua unataka aache, ajenge kwakua anataka na si kwakua unataka, kama unataka maendeleo fanya wewe.
Wengine sasa utasikia nilimkuta hana kitu nikamshauri akajenga, kaacha pombe, sasa kawa mzuri kaniacha. Dada yangu kwani ilikua ni lazima akuoe, umemfanya mtu mwema sawa lakini bado atakuona kama kisirani tu. Atawaza huyu mwanamke ana mawazo mazuri lakini ana kisirani hafai kuwa mke, hivyo shauri lakini acha kulazimishia mambo, kama unaona ushauri wako ni mzuri ufanyie kazi wewe!
Comments
Post a Comment